Tuesday, July 24, 2007

SHESHE LA UJAMBAZI BONGO!!!


Na Wandishi Wetu, Arusha, Dar, Dodoma
Mapambano kati ya vyombo vya usalama nchini na majambazi yaliyotokea Arusha wiki iliyopita hayajawahi kutokea. Kauli hiyo ilitolewa na baadhi ya watu walioshuhudia mapambano kati ya polisi, wanajeshi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Usalama wa Taifa ambapo majambazi mawili yalirushiana risasi na wanausalama hao.

UWAZI ambalo lilikuwa katika eneo la tukio huko Njiro, mjini Arusha lilishuhudia ‘vita’ hiyo ambapo baadhi ya polisi waliozungumza nasi walisema walielekezwa kutoka ngazi za juu ya jeshi la polisi kutowaua watuhumiwa hao wa ujambazi wakati wanashambuliana.

Katika mapambano hayo silaha kali kama vile RPG, mabomu ya mikono, bunduki za rashasha zilionekana zikitumia ambapo pia mabomu ya machozi takribani 20 yalilipuliwa eneo hilo. Kwa mara ya kwanza polisi na viongozi wa serikali walionekana wakiwa wamevaa jaketi maalum za kuzuia kupenya risasi kama vile Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Kapteni Evance Balama ambaye kitaaluma ni askari.

Habari za ndani kutoka jeshi la polisi zinadai kuwa wasichana wawili ambao majina yao hayakuweza kutolewa hadharani walisaidia kuweza kupatikana kwa watu hao. Wasichana hao bado wanashikiliwa na vyombo vya usalama. Watuhumiwa waliokamatwa ni Samuel Gitau Saitoti ambaye ni Mkikuyu, mkazi wa Ngong Nairobi na Peter Michael Kimenya mkazi wa Thika, Nairobi Kenya.

Aidha polisi pia juzi katika eneo la Nguleto walimtia mbaroni Samsoni Chonjo anayedaiwa kuwa kundi moja na waliokatwa siku ya tukio la kurushiana risasi. Katika ukaguzi wa polisi ndani ya jumba ambalo watuhumiwa walikuwa wamejifungia jumla ya shilingi 978,000 na dola za Kimarekani 8,145 zilikutwa.

Aidha mabomu ya kurushwa kwa mkono, bastola tano na bunduki aina ya Semi Automatic Rifle (SMG) mbili zilikamatwa pamoja na risasi 85. Tayari maofisa wa polisi kutoka Makao Makuu ya jeshi, mkoa wa Kilimanjaro na wa Arusha wapo mjini hapa wakiwahoji watuhumiwa hao.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Bw. Basilio Matei alipohojiwa kuhusiana na watuhumiwa hao alisema bado wanahojiwa.

“Bado tunawahoji kuhusiana na matukio ya ujambazi na sio lile la Mwanga tu,” alisema Bw. Matei akimaanisha kuwa licha ya watuhumiwa kutuhumiwa kuiba zaidi ya shilingi mjilioni 200 katika Benki ya Microfinance (NMB) mjini Mwanga, wanataka kujua pia mambo mengine ya kihalifu kama walihusika nayo.

Mwandishi wetu alizungumza na Mwenyekiti wa Mtaa wa Korongoni Zulfa Mhina ambako ndiko tukio lilipotokea aliyebainisha kuwa siku za nyuma aliwaona watuhumi wakiwa wanawatafutia wenzao nyumba za kupanga katika eneo lake.

Alisema mtu mmoja alifika nyumbani kwake na kudai kuwa ana vijana kutoka nje ya nchi ambao walikuwa wakitafuta nyumba ya kupanga na baadaye akapata taarifa kuwa nyumba iliyofanyika tukio imepata wapangaji.
Alifafanua kuwa alipewa taarifa hiyo na aliyekuwa mlinzi wa nyumba hiyo Bw. Hamisi Kironga ambaye hata hivyo aliondolewa baada ya majambazi hayo kupanga. Tukio hilo lilimfanya Mbunge wa Arusha, Mhe. Felix Mrema kukatisha kuhudhuria kikao cha bunge na kuja mjini hapa na alikuwa mmoja wa viongozi waliokuwa pamoja na polisi na wanajeshi waliokuwa wakitafuta mabomu katika nyumba waliyokutwa watuhumiwa.

Wakati huo huo Jijini Dar es Salaam, mkoa wa kipolisi wa Kinondoni mtu mmoja anayetuhumiwa kwa ujambazi amekamatwa. Kamanda wa Polisi wa mkoa huo Bw. Jamal Rwambow amelithibitishia gazeti hili kukamatwa kwa mtu huyo aliyemtaja kwa jina la Omari Salum na mwenzake Rashid Fumo, alisema wanahojiwa na jeshi lake.

Matukio ya ujambazi yamepamba moto sehemu mbalimbali nchini baada ya kutulia kwa kipindi cha mwaka mmoja na miezi sita. Juzi Waziri wa Usalama wa Raia, Mhe. Bakari Mwapachu alizungumza na wandishi wa habari mjini Dodoma ambapo aliwashukuru wananchi kwa kutoa ushirikiano katika vita dhidi ya majambazi.

Alimuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini. Bw. Saidi mwema kuimarisha mazungumza na mwenzake wa Kenya ili kuthibiti hali hiyo kwani alisema majambazi wengi wanatoka huko na wanashirikiana na baadhi ya Watanzania.

MGANGA ALIYE WEKA KUFULI
Na Mwandishi wetu, Kibaha
Mganga wa kienyeji, Bibi Catherine Punde Kadede (70) mkazi wa Msangani Wilaya ya Kibaha ambaye anadaiwa kumuweka kufuli sehemu za siri mwanamke mmoja ili apate mimba hatimaye kuzaa ameanikwa hadharani.

Aliyemuanika hadharani ni Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani, Bw. Henry Salewi alipoongea na waandishi wa habari ofisini kwake wiki iliyopita ambapo alisema mganga huyo alikuwa akimtibia mgonjwa wake aitwaye Halima Mohamed ambaye alienda kupata tiba baada ya kuishi kwa miaka miwili na mumewe bila ya kupata mamba.

Mwanamke huyo ni mkulima wa eneo la Jamaika Kwa Mathiasi na alikwenda kwa mganga huyo akitaka apatiwe dawa ili aweze kupata mtoto baada ya kutopata mtoto kwa kipindi hicho alichoishi na mumewe.

Akielezea Salewi alisema tukio hilo lilitokea Julai 16 mwaka huu majira ya saa 3 asubuhi katika kijiji cha Msangani. Alisema Mwanamke huyo alkwenda kwa mganga huyo akiwa na mumewe Shabani Lamji ambaye kazi yake ni mchimba visima.

Alifafanua kuwa walipofika kwa mganga huyo na kumweleza matatizo yao, mwanamke alitakiwa kuweka punje 10 za kunde na maharage na kasha akamtumbukiza kufuli ukeni.

"Wanandoa hao waliondoka baada ya kupewa dawa za kunywa mwanamke na baada ya kuzitumia mwanamke yule alipata maumivu makali lakini alivumilia kwakuwa ndiyo dawa zenyewe lakini hakupata mabadailiko yoyote zaidi ya maumivu makali," alisema Salewi.

Alisema dada huyo alipata maumivu makali akamwambia kuwa anamuumiza akamjibu kwa kuwa unashida ya mtoto avumilie na alipomuuliza juu ya kufuli kuwa litatokaje alimjibu kwamba yeye ndiye mtaalamu hivyo asihofu.

Salewi amesema punje za maharage na kunde hazikuweza kuingia kwani zilizuliwa na kufuli na kuanguka akaambiwa hiyo ni dawa tosha na atafanikiwa kupata mtoto.

Akaongeza kuwa mwanamke alivumilia kwa siku mbili akaona maumivu yanazidi akaenda kituo cha polisi Kwa Mathias na kutoa taarifa na na kupewa PF 3 kwa ajili ya kupatiwa matibabu kwenye hospitali ya Tumbi.

"Mdakatari walimtoa kufuli ile na kumwanzishia matibabu na hadi sasa anaendelea kupata tiba hospitali hapo,"aliongeza Salewi.
Mganga huyo alimekamatwa na polisi wanaendelea na upelelezi.


No comments: