Sunday, July 15, 2007

KUPIMA NGOMA MCHEZO?


Ijumaa Wikienda liko mitaani Jumatatu hii kama linavyoonekana, Mzimu wa hayati Amina Chifupa bado ungalipo...nae Miss Universe wa Bongo aanguka ghafla akiwa kwenye foleni ya kupima 'ngoma' jamani....! PATA HABARI KAMILI ........

Makongoro Oging' na Jimmy Mfuru
Katika hali iliyotafsiriwa kama ni usanii ili kukwepa kupima Virusi Vya Ukimwi, Miss Universe Tanzania 2007, Flaviana Matata, alidondoka chini kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam, wakati akisubiri zamu yake ifike ili naye atolewe damu kwa ajili ya kupimwa 'ngoma'.

Tukio hilo lililotafsiriwa kama sinema, lilitokea Jumamosi iliyopita, wakati wa kampeni ya kitaifa, kuhamasisha upimaji wa virusi ukimwi ambapo Flaviana alianguka akiwa nje ya banda alimoingia Rais Jakaya Kikwete, kuzindua rasmi zoezi hilo.

Mrembo huyo aliyekuwa bega kwa bega na meneja wake, Maria Sarungi, mwanzoni hakuwa na woga, lakini hali ilibadilika wakati alipokuwa akifuatilia zoezi la rais kupima virusi litakavyokwisha.

Kamera yetu ambayo ilikuwa ikimmulika Flaviana nukta baada ya nukta, iliweza kuona mabadiliko usoni mwake na mara nyingi mrembo huyo alikuwa akiteta mambo fulani na meneja wake.

Aidha, wakati watu wengi wakingoja majibu ya rais yatolewe, ghafla Miss Universe huyo alianguka, kitendo ambacho kilimshtua kila mtu aliyekuwa jirani yake huku wengine wakidai kwamba mrembo huyo alifanya usanii makusudi ili asipime.
"Kupima ngoma unafikiri mchezo jamani! Huyu dada ni mjanja, kaona kupima ukimwi ni 'ishu', halafu ukizingatia yeye ni 'supastaa' ndiyo maana kajiangusha." alisikika jamaa mmoja aliyeshuhudia 'sinema' hiyo.

Mwanamke mwingine aliyeshuhudia mkanda huo alisema: "This is an art (hii ni sanaa), huyu Flaviana ni mjanja sana, amejiangusha ili asipime tu, hakuna kingine."
Hata hivyo, pamoja na idadi kubwa ya watu kuamini kuwa Flaviana alicheza 'muvi' kuanguka, lakini kuna baadhi walimhurumia.

"Maskini dada wa watu, yamemkuta yapi tena na kuanguka? tusijekuanza kampeni hizi kwa msiba," alisikika dada mwingine ambaye alionekana kulengwa na machozi.
Baadaye, wasamaria wema, akiwemo Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe kwa kushirikiana na Maria Sarungi, walimbeba Flaviana na kumpeleka katika jukwaa alilolitumia rais kuhutubia siku hiyo na kumpatia huduma ya kwanza.

Aidha, baada ya kupewa huduma hiyo, mrembo huyo aliamka huku akionekana amelegea kabla ya watu wa msalaba mwekundu (Red Cross) kufika eneo la tukio na kumpakia kwenye gari, kumuwahisha hospitali kwa uchunguzi zaidi.

Akiongea kwa simu na gazeti hili, Maria Sarungi, alisema kuwa chanzo cha kuanguka ghafla kwa mrembo huyo kilitokana na kusimama kwa muda mrefu juani na kwamba alikuwa hajisikii vizuri kabla hata ya kufika hapo.

Alisema, kutokana na hali hiyo ilibidi amlazimishe mnyange huyo kuhudhuria uzinduzi huo wa kupima 'ngoma' kwa sababu Flaviana alikuwa ni mmoja wa waalikwa.
"Tangu asubuhi alikataa kuhudhuria kampeni hiyo kutokana na kujisikia vibaya, lakini nilimlazimisha, kwa sababu tulikuwa hatuna budi kuhudhuria kutokana na kupewa mwaliko rasmi," alisema Sarungi.

Hata hivyo, daktari mmoja maarufu kutoka hospitali moja kubwa jijini Dar es Salaam alisema kuwa tukio la Flaviana lilitokana na kukumbwa na hofu ya tukio kubwa lililokuwa mbele yake.

Daktari huyo (jina tunalihifadhi kwa sababu maalumu) ambaye ni mmoja wa waliomshuhudia mrembo huyo akianguka siku hiyo, alisema, hali hiyo kitaalamu inaitwa 'Neuro Genic Shock'.

"Huo ni mshtuko uliotokana na hofu, inavyoonekana alikuja hapa (Mnazi Mmoja) bila kujiandaa kisaikolojia, kwahiyo kama nikipewa nafasi ya kumshauri, nitamwambia siku nyingine asiende kwenye tukio kubwa kama hili au zaidi bila kufanya maandalizi ya kutosha kisaikolojia," alisema daktari huyo.

Katika uzinduzi wa kampeni hiyo, Rais Kikwete alisema, wananchi wasione aibu, bali wajitokeze kwa wingi kupima afya zao na kuwaasa wananchi kuacha tabia ya kuwanyanyasa wagonjwa wa ukimwi, badala yake wawaoneshe mapenzi makubwa.
"Ugonjwa huu ni hatari kwa kila mmoja labda itokee tu huyo mtu hashughuliki ama mambo yake siyo mazuri' alisema Rais Jakaya.

2 comments:

Anonymous said...

Mh Abdallah Mrisho, nakumbuka siku ya kwanza ulipoanza kutundika news za magazeti ya udaku uliahidi kwamba ungekuwa unaweka news kamili kwenye blog yako. Na ulifanya hivyo kwa siku 2 za mwanzo, baada ya hapo naona umegeuza blog yako kuwa ubao wa matangazo ya headlines za magazeti ya udaku. Lengo lako lilikuwa kuongeza watembeleaji wa blog yako au ulikuwa na agenda gani?

It is better kuwa mkweli badala ya kutumia hila za kudanganya watu kwamba utakuwa unawapa news hizo na ghafla unaanza kutuwekea headlines. Haina maana yoyote kuweka headlines kwenye blog wakati watu unaowawekea hayo matangazo wako nje ya Tanzania na hawawezi kununua gazeti husika hata kama wangetamani kusoma news za kwenye hilo gazeti.

Naomba uweke wazi ili watembeleaji wa Blog yako tujue kama unaendelea na headlines ama utaweka news kamili. Hii itapunguza lawama na wala mtu hawezi kupoteza muda kuingia kwenye blog yako kama anajua kwamba akija atapata news nusu na kumuacha akiwa na maswali mengi bila majibu! Ni maoni tu na samahani kama utakuwa umekereka, lakini ukweli lazima uambiwe.

Anonymous said...

Ndugu Mrisho au Meneja wa Global sasa ulituambia kwa sie tulioko nje ya nchi twaweza soma gazeti lenu live kupitia hii blog yako,na ukatuhamasisha tuwaambie na wengine na tukajitahidi kuitangaza blog yako,hee mara siku mbili ndo tumesoma habari hizo,bada ya hapo naona ni vichwa vya habari tu,au ulikuwa unatangaza blog?nisamehe kama nimekukera.Ila jua ya kwamba kwa sie tulio nje ya Tz hatuyapati hayo magazeti yenu.