Tuesday, March 10, 2009

Epuka ugonjwa wa moyo kwa kula hivi:


KILA mara tunasisitiza kuwa chakula ndiyo kila kitu katika maisha yetu, pale tunapokitumia vizuri kinatuletea faida na pale tunapokitumia vibaya hutuletea madhara makubwa katika afya zetu, yakiwemo matatizo ya ugonjwa wa moyo.

Utafiti uliofanywa nchini Marekani hivi karibuni, unaonesha kuwa, takriban Wamarekani Milioni 9 wanasumbuliwa na ugonjwa wa moyo na unaua mtu mmoja kila baada ya sekunde 37! Sijajua hali ikoje nchini Tanzania.

Ili kujiepusha na hatari ya kupatwa na ugonjwa wa moyo, mambo 10 yafuatayo hayana budi kufuatwa na kuzingatiwa:

KIJUE KIWANGO CHAKO CHA KOLESTRO
Kwa kawaida binadamu tuna mafuta mwilini yanayojulikana kitaalamu kama ‘High-density Cholesterol (HDL), Low-Density Cholesterol (LDL) na Triglycerides (TG). ‘LDL’ na ‘Triglycerides’ ni mabaya na hasa ukiwa nayo mengi mwilini, ndiyo huwa chanzo cha ugonjwa wa moyo. Hivyo ni vyema ukaenda kwa Daktari na kujipima afya yako.

JIJUE UKO KATIKA HATARI KIASI GANI
Utakuwa uko katika hatari ya kupata ugonjwa wa moyo iwapo utakuwa na matatizo ya presha, kiwango kikubwa cha mafuta mabaya ya kolestro na ukawa unavuta sigara pia. Wataalamu wetu wanatuambia kuwa matatizo hayo yana muongezea mtu hatari ya kupata ugonjwa wa moyo mara nane zaidi katika kipindi cha miaka sita ijayo, hivyo epuka uvutaji sigara.

PUNGUZA UZITO
Kupunguza uzito, hata kwa kilo 5, ni jambo la lazima iwapo unataka kujiepusha na magonjwa ya moyo. Uzito mkubwa sana ndiyo huwa chanzo kikuu cha magonjwa ya kisukari, shinikizo la damu ambayo hatimaye huweza kusababisha ugonjwa wa moyo.
PUNGUZA ULAJI WA MAFUTA
Vitu kama siagi, krimu, ‘mayonaizi’ na vipande vya nyama vyenye mafuta ni miongoni mwa yale mafuta mabaya (“bad” LDL cholesterol), ambayo huchangia kwa kiasi kikubwa uzibaji wa mishipa ya damu (arteries) mwilini, hivyo epuka ulaji wa vitu hivyo kwa wingi. Badala yake kula mafuta yatokanayo na mboga, kula samaki au nyama ya kuku isiyokuwa na mafuta.

ACHANA NA VYAKULA VYA MAKOPO
Kwa kawaida vyakula vya makopo huwa na mafuta na chumvi nyingi pamoja na kemikali nyingine za kuhifadhia chakula ambavyo huchangia mlaji kuwa na mafuta mabaya mengi mwilini. Ununuapo vyakula kwenye makopo, lazima usome na ujue vilivyomo kabla ya kuamua kutumia.
KULA VYAKULA VYENYE ‘Fiber’
Kwa Kiswahili ‘fiber’ inajulikana kwa jina la ‘ufumwele’ ambao ni muhimu sana kwa ustawi wa moyo. Tunashauriwa kula vyakula vyenye kiwango kikubwa cha ufumwele, kama vile maharage, kunde, n.k pamoja na matunda jamii ya machungwa.

KULA NAFAKA HALISI
Badala ya kupenda kula vyakula vilivyotengenezwa kutokana na nafaka zilizokobolewa, ambazo huwa chanzo cha magonjwa kama kisukari na presha, kama vile mkate au ugali mweupe, pendelea kula sembe, dona au mkate mweusi ambao husaidia kuondoa mafuta mabaya mwilini na huepusha magonjwa ya kisukari.

KULA SAMAKI
Utafiti unaonesha kuwa mtu akila samaki, angalau mara mbili kwa wiki, anajiepusha na hatari ya kupatwa na ugonjwa wa moyo kwa asilimia 30 zaidi. Samaki wana mafuta aina ya Omega-3 ambayo hupunguza kiwango cha mafuta mabaya mwilini yanayosababisha kuziba kwa mishipa ya damu. Pia Omega- 3 hupunguza kiwango cha presha ya damu mwilini.

KULA ‘NJUGU’
Utafiti mwingine unaonesha pia kuwa watu wanaopenda kula ‘njugu’, kama vile karanga, korosho ,n.k, kwa wiki mara mbili au nne, wana uwezekano mdogo sana wa kupatwa na magonjwa ya moyo kuliko watu wasiokula. ‘Njugu’ zina aina nzuri ya mafuta kwa afya ya moyo.

‘KUNYWA’ KIASI
Utafiti wa kisayansi unaonesha kuwa wanywaji kiasi wa kilevi, wana uwezekano mdogo wa kupatwa na ugonjwa wa moyo kuliko wasiokunywa kabisa. Kilevi- hasa wine- kinasadikika kuifanya damu kuwa nyepesi na kuongeza mafuta mazuri mwilini (HDL Cholestrol).

Zingatia mambo hayo 10 na moyo wako utakuwa salama!

4 comments:

Yasinta Ngonyani said...

Asante kwa somo hili nzuri. Maana ni kweli vizuri kujua ni vyakula gani tule sio kuvamia tu

Anonymous said...

Mdau Maybe08

Sasa kaka Mrisho unataka kupigwa kibao kama mze Ruksa yaani unataka tuanze kuonja kilevi na dini zote zinakataza?(joks)

Tunashukuru kwa somo lako zuri kwakweli unatusaidia sanaaa sanaa yaani mungu ndiye atajuwa namna ya kukulipa kwa jinsi unavyookoa watu kwa kuwafundisha namna ya kutunza afya zao, ni thawabu SHUKRANI SANA.

LAKINI bado hujanijibu swali langu nilikuomba kitaambo msaada wa jina la ULEZI aina ya nafaka kwa lugha ya kigeni (english) nitashukuru zaidi

Mrisho's Photography said...

Mdau Mayb08: Ulezi kwa 'kidhungu' unajulikana kama 'millet flour' ama'finger millet flour'....usinipige kofi na mimi, mambo mengine tuvumiliane jamani..teh teh!!!

Anonymous said...

Maybe08

Well, well Bro! Nashukuru na nimefurahi sana tena sana kwa msaada wako M/mungu akuzidishie afya njema na uhai mrefu utusaidie hili na jingine


Mdau USAgara