

Tuzo za muziki Tanzania 2008/2009: UVUNDO UMEENDELEA
Na Mwandishi Wetu
Kama kawa, Kamati ya Tuzo za Muziki Tanzania, imerudia kasoro za upangaji wa vipengele vya muziki na wasanii walioteuliwa kuwania ‘awadi’ hizo kwa msimu wa mwaka 2008/09.
Kilele cha utoaji wa tuzo hizo, kilifanyika usiku wa Jumamosi iliyopita kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee na kushuhudia mambo ambayo ni rahisi kuyaita uvundo.
Kipimo cha kwanza kinachosherehesha uvundo huo ni ushamba mkubwa wa kushindwa kutambua aina ya muziki na wasanii wake, hivyo kutengeneza makundi (category) yaliyojaa upungufu.
Katika utoaji wa tuzo hizo, kulikuwa na makundi 20, lakini udhaifu mkubwa ulijionesha katika kundi la pili, 11, 12 na 18.
Udhaifu wa category ya pili lililokuwa na wateuliwa wa Tuzo ya Mwimbaji Bora wa Kiume, lilishindwa kukidhi haja kwa kuwajumuisha wasanii Matonya, Makamua, MB Dog, Hammer Q na Q- Jay pekee.
Kamati ilishindwa kutambua uwepo wa mwanamuziki aliyetia fora mwaka jana, Lawrence Malima ‘Marlaw’ ambaye alivuma na nyimbo kadhaa, lakini kwa mshangao wa wengi hakuteuliwa kuwania tuzo hiyo.
Kasoro ya Kundi la 11 ni kuzijumuisha nyimbo Nipe Deal wa Albert Mangwea ‘Ngwair’ na Nakuita Njoo wa Joseph Haule ‘Prof Jay’ katika category ya Wimbo Bora wa Hip Hop, wakati ala zake hazipo kwenye aina hiyo ya muziki.
Kitendo cha kamati kuziweka nyimbo Taxi Bubu wa Seif Shaaban ‘Matonya’ na Mama Neema wa Hamis Kinzasa ‘20%’ katika category ya Wimbo Bora wa Reggae/Ragga kilisababisha kasoro kubwa kwenye Kundi la 12.
Kimsingi nyimbo hizo mbili hazipo kwenye staili hiyo ya muziki.
Kundi la 18 lilionesha kuwa kamati bado ina ushamba wa kutokujua aina ya muziki kwa sababu ya kasoro moja ya kuiweka traki ya Kassim Maganga inayoitwa Awena katika category ya Wimbo Bora wa Zouk, wakati midundo yake haipo kwenye mahadhi hayo.
KULIKUWA NA TUZO FEKI
Khadija Shaaban ‘Keisha’ ni mwanamuziki mzuri, lakini kitendo cha kubeba tuzo ya Mwimbaji Bora wa Kike mbele ya mkali, Judith Wambura ‘Lady Jaydee’, Mwasiti Almasi na Isha Ramadhani ‘Mashauzi’ haikuwa sawa.
Keisha hakufanya kazi kubwa mwaka jana, ya kumfanya awapige kumbo akina Jaydee, Mwasiti na Isha Mashauzi ambao waliweza kutawala vyombo vya habari vilivyo.
MB Dog, hakupaswa Tuzo ya Mwanamuziki Bora wa Kiume kwa sababu alifunikwa mno mwaka jana. Marlaw, Matonya na Hammer Q kama si siasa zilizopo, walistahili.
Tuzo ya Wimbo Bora wa Reggae/ Ragga kwenda Tunda Man kupitia traki yake Ripoti haikuwa sawa. Kamati ilishindwa kuwachukua wanamuziki halisi wanaoimba staili hiyo kama Jah Kimbute, Jhikoman, Innocent Nganyagwa na wengineo.
JOHN DILINGA AOMBWA KUJIUZULU
Watu wanatambua kuwa John Dilinga ‘JD Mat Lou’ ni mdau wa muziki na anaujua vizuri, lakini tatizo ni wajumbe anaowaongoza katika Kamati ya Tanzania Music Awards.
JD ndiye mwenyekiti, lakini wajumbe wengi waliopo kwenye kamati hiyo bado wana kasoro katika kuujua muziki. Hiyo ndiyo sababu ya matatizo yaliyopo, hivyo ameombwa na wadau ajiuzulu ili asiendelee kuchafuka.
ZOMEA ZOMEA ILIKUWEPO
Wakati wa utoaji wa tuzo, kulikuwa na hali fulani ya zomea zomea kwa baadhi ya watu walioonekana kuchemsha. Kubwa zaidi ni kwa Mwenyekiti wa Yanga, Iman Madega, hali hiyo ilimkuta alipoanzisha mjadala wa Usimba na Uyanga ukumbini, wakati alitakiwa kumkabidhi Dogo Mfaume, Tuzo ya Wimbo Bora wa Asili ya Kitanzania aliyoshinda kupitia traki yake, Kazi ya Dukani.
Miss Tanzania 1999-2000, Hoyce Temu naye alijikuta akizomewa, baada ya kuonekana anataka kuchelewa kumtaja mshindi wa Tuzo Bora ya Wimbo wa Afrika Mashariki. Mrembo huyo alitoa maelekezo ya kutaka waliokuwa wanashindania ‘awadi’ hiyo waoneshwe kwanza, wakati zoezi hilo lilikuwa limekwishafanyika.
TUZO ZILIKUWA HIVI
Mwimbaji Bora Kike (Keisha) wa Kiume (MB Dog) Albamu ya Taarab (VIP, Jahazi) Wimbo wa Taarab (VIP, Jahazi) Wimbo wa Mwaka (Anita, Matonya) Wimbo wa Kiswahili (Heshimwa kwa Mwanamke, Akudo Impact) Albamu ya Kiswahili (Pekecha Pekecha, Akudo).
Wimbo wa R&B (Natamani, Wakali Kwanza) Wimbo wa Asili ya Kitanzania (Kazi ya Dukani, Dogo Mfaume) Albamu ya Asili ya Kitanzania (Dela Dela, Chemundugwao) Wimbo wa Hip Hop (Ngoma Itambae, Chid Benz) Wimbo wa Reggae/Ragga (Ripoti, Tunda Man).
Msanii wa Rap (Ngwea) Wimbo wa Afrika Mashariki (Salary, Nameless) Mtunzi wa Muziki (Karama Legesu) Mtayarishaji wa Nyimbo (Hermy B) Mwandikaji Bora (Prof Jay) Wimbo wa Zouk (Nalivua Pendo, Mwasiti) Mtayarishaji wa Video (Kallage Pictures) Wimbo wa Kushirikiana (Anita, Matonya na Lady Jaydee).
**************

Miongoni mwa wasanii wachache wa muziki wa Bongo Flava ambao hawafichi dili walizowahi kupiga kabla hawajatoka kunako game ni pamoja na Mohamed Ally a.k.a Z-Anto ambaye hivi karibuni alitamka kwamba, yeye ni fundi mzuri wa kutengeneza majiko.
Akipiga stori ndani ya kipindi cha ‘Nani ni nani’ kilichoasisiwa na Frank Mtao na kurushwa hewani kupitia Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, msanii huyo anayeunda familia ya Tip Top Connection alisema kwamba kabla hajatoka kupitia muziki alikuwa akipiga dili mbalimbali za sanaa ikiwemo hiyo ya kutengeneza majiko.
“Nakumbuka siku moja nilipokuwa Nairobi kwenye shoo, nilikatiza kwenye mtaa fulani nikakuta kuna sehemu watu wanatengeneza majiko kwa kutumia mabati magumu, nikavutiwa ikabidi niwaombe nijaribu. Huwezi kuamini, nilitengeneza jiko zuri mpaka wakabaki wanashangaa kwasababu walidhani mimi ni muziki tu,” alisema Z-Anto ambaye hivi karibuni atadondosha video ya wimbo wake mpya, ‘Peace & Love’ aliyowashirikisha Pingu na Juacali kutoka Kenya.
************************************

Hakuna shabiki wa muziki asiyefahamu kwamba msanii Lucas Mkenda a.k.a Mr. Nice kuwa aliwahi kuitikisa Afrika Mashariki kwa ngoma zilizowapagawisha wengi, hata mitaani kwetu na sehemu nyingine tulipokuwa tukikatiza tulikutana na baadhi ya watoto wakiimba nyimbo hizo kama Kikulacho, Kidali po na nyingine.
Tunachotaka kusema ni kwamba, baada ya kupotea kwa muda mrefu kwenye game huku akiwaacha mashabiki wake njia panda, mchizi amerudi tena, mkononi akiwa na albamu yenye jina la ‘Wakinuna’ ambayo ina jumla ya nyimbo saba itakayozinduliwa Aprili 12, mwaka huu ndani ya Ukumbi wa Maisha Club uliopo jijini Dar es Salaam.
Swali ambalo liko vichwani mwa mashabiki na wadau wengi wa burudani Bongo, ni je, Mchizi ataweza kusimama kama enzi zile za ‘Kidali po’ au ‘Kikulacho?
**********************************

Staa wa muziki wa R&B Marekani, Jennifer Hudson ndiye tunamcheki leo kupitia ‘Ebwana Dah!’ yakiwa ni maombi ya baadhi ya wasomaji waliopenda kufahamu mwanadada huyo mwenye umbo kubwa na anayekimbiza kunako game ya muziki duniani hivi sasa, amewahi kujiachia na mastaa wa kiume wangapi.
Kwa mujibu wa mtandao unaodili na ishu hizo, James Peyton ndiye aliyeanza kutoka na Jennifer mwaka 1999 hadi 2004 na kumuachia David Otunga ambaye aliripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa alikuwa na mpango wa kuchukua jumla (kuoa) baada ya kumvalisha pete ya uchumba, ndoto ambazo ziliyeyuka ghafla na mwaka 2007 wakatosana.
Kilichofuata baada ya hapo, Jennifer aliamua kujiweka kwa Kerry Rhodes na haijafahamika mara moja kama bado yuko naye hadi hii leo. Kwa kifupi hao ndiyo mastaa wa kiume waliowahi kujirusha na Jennifer Hudson ambaye hivi sasa ana umri wa miaka 27.
Staa huyo ambaye jina lake kamili ni Jennifer Kate Hudson mwenye nywele nyeusi na macho ya dark brown alizaliwa Septemba 12, 1981 huko Chicago, Illinois, Marekani.
credits: MC George, R. Bukos
2 comments:
Kwanza, ahsante sana kwa habari moto moto hasa zinazohusu afya.
Pili, Tafadhali unapopata habari toka hiyo website uwe unazifanyia kazi kidogo kama kutembelea tovuti za mhusika au google jina lake upate ukweli, nasema hivyo sababu jenniffer hudson, bado ni mchumba wa David Otunga na wanaplan harusi yao.
mtembelee hapa :-
www.jennferhudsononline.com
Yes i like her big boo too,
Huyu jamaa siyo kwa jennifer peke yake ma-star kibao tu waliopita ana mention guys waliokuwa nao lakini wengi wao sivyo most of them ni katika kazi and not athorwise!
Post a Comment