Thursday, April 29, 2010

Ijue siri ya kinga ya mwili


Kwa kawaida, kila mwili wa binadamu una kinga ya mwili ya asili ambayo kazi yake ni kupambana na bakteria, parasiti, virusi na vitu vingine vinavyosababisha maradhi mbalimbali, ukiwa ni uumbaji wake Mungu mwenywe.

Vitu hivyo, ambavyo vimo ndani ya miili yetu, kila siku hujitahidi kuushambulia mwili kwa njia moja ama nyingine, lakini kinachofanya jitihada zao zigonge mwamba, ni kinga ya mwili aliyonayo mtu.

Kwa mantiki hiyo, mtu anaye ugua mara kwa mara, bila shaka huyo kinga yake ya mwili ni dhaifu na yule ambaye haugui mara kwa mara, kinga yake inaonesha iko imara. Kazi ya kinga ya mwili ni kuwazuia wavamizi wapya na kuwadhibiti waliokwisha ingia mwilini wasilete madhara.

Tunaposema mtu mwenye kinga dhaifu haishi kuugua mara kwa mara, tuna maanisha kuugua magonjwa mbalimbali, yakiwemo yale yanayoweza kuonekana madogo kama mafua, homa, kutoka vipele sehemu za siri, kuumwa ‘tonsi’ na kuumwa magonjwa makubwa ya saratani.
KINACHOSABABISHA KINGA DHAIFU
Kuna vitu vingi vinavyoweza kusababisha kinga ya mwili kuwa dhaifu, miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na mtu kuwa na mawazo mengi, mfadhaiko wa akili, kuishi staili mbovu ya maisha, ulaji mbaya na ukosefu wa virutubisho mwilini.

Aidha, inaelezwa kuwa mambo mengine yanayosababisha kudhoofika kwa mfumo wa kinga ya mwili, ni HIV, saratani, upungufu wa chembechembe za damu nyeupe na matumizi ya dawa za hospitalini kwa muda mrefu. Vile vile upungufu wa kinga unaweza kusabishwa na umri mkubwa, halikadhalika kinga ya mwili kwa watoto wadogo na mama wajawazito huwa chini.

JINSI YA KUKABILIANA NA TATIZO KIASILI ZAIDI
Kutegemeana na chanzo cha tatizo lako, ulaji wa lishe nzuri yenye virutubisho vyote muhimu, kunaweza kudhibiti tatizo kwa haraka zaidi. Licha ya lishe, pia unaweza kutumia vidonge vya lishe (food supplements) au vidonge vya asili vya aina mbalimbali ambavyo vimetengenezwa maalum kwa kuongeza kinga mwilini.

KUONGEZA KINGA KWA NJIA YA LISHE
Ni ukweli ulio wazi kuwa, njia bora na ya kipekee ya kukabiliana na ukosefu wa kinga mwilini, ni kula mlo wenye virutubisho vyote muhimu. Hivyo, inashauriwa mlo wako uwe kwa kiasi kikubwa ni wa vitu vifutavyo:

Hakikisha unakula kwa wingi matunda, mboga za majani, nafaka lishe, maharage na karanga, epuka kula kwa wingi sukari, hasa nyeupe. Pia kula vyakula kwa wingi kama machungwa, karoti, viazi vitamu, nyanya na pilipili mboga bila kusahau jamii zote za kabichi.

MAJI NA MAZOEZI
Kuimarisha ufanisi wa kinga yako ya mwili, hakikisha unakunywa maji ya kutosha kila siku, kiasi kisichopungua glasi 10- 12 na kufanya mazoezi ya mara kwa mara. Maji ni muhimu sana, kwani ndiyo yatakayokusaidia kutoa sumu mwilini kwa njia ya mkojo na mazeozi yatatoa kwa njia ya jasho.

Jiepushe na kufanya kazi au kukaa katika mazingira yanayokusababishia ‘stress’ na badala yake pumzika au tembelea mahali ambako kutapumzisha akili yako na kukupa faraja moyoni, jiepushe kuishi maisha ya wasiwasi na hasira, yanauwa kinga yako ya mwili!

2 comments:

Disminder orig baby said...

siku nyingi sikupita kijiwe changu kaka. Asante sana upo karibu na ukweli kabisa.

Unknown said...

Mh yupo karibu na ukweli he INA maanisha ukweli hajaufikia katika maelezo yake nakama hajaufikia ukweli INA maana muongo au kuna maana nyingine ya maneno yako kiongozi???
Binafsibna shkuru somo zuri saana