Tuesday, June 15, 2010

Unajua kwanini tunaugua mara kwa mara? - 3

Wiki iliyopita tulianza makala haya yenye lengo la kujua sababu za watu kuugua mara kwa mara. Tumeanza kwa kuona kuwa mwili una kanuni zake ambazo ni lazima zifuatwe na zisipofuatwa huleta maradhi. Vile vile tumeona kuwa maradhi hayaji ghafla, bali huanza kwa kutoa ishara ambazo watu wengi, ama hawazijui au huzipuuzia…Sasa endelea.

Hakuna njia nyingine ya kuwawezesha isipokuwa kula vyakula sahihi ambavyo vitatoa virutubisho vinavyohitajika mwilini. Unapokula vyakula vyenye virutubisho ‘walinzi’ wako hufurahi na hupata nguvu zaidi za kukulinda

Vyakula gani ni sahihi?
Katika jeduari la chakula (food Pyramid), vyakula vya nafaka ndiyo vinaonesha kuchukua sehemu kubwa kuliko vyakula vingine. Tunatakiwa kula kwa wingi vyakula vitokanavyo na nafaka zenye viini lishe vyake. Mathalan, unapokula ugali utokane na mahindi yenye viini lishe.

Tunapokunywa uji tunywe unaotokana na nafaka ambayo haijakobolewa. Tunapokula mkate, tunatakiwa tule uliotengenezwa kwa ngano isiyokobolewa, hivyo hivyo kwa vyakula vingine vitokanavyo na mtama, ulezi, mpunga, n.k. katika kundi hili kuna viazi vitamu, korosho pamoja na tambi.

Kundi hili la vyakula ndiyo namba moja na ndiyo ambalo tunatakiwa kula vyakula vyake kwa wingi kila siku, bila kusahau kunywa maji mengi, kama tulivyosema, walau glasi nane kwa siku, kama huna kazi ngumu, lakini kama una kazi ngumu unatakiwa unywe zaidi ya hapo.

Soma kwa makini makundi haya ya vyakula na kiwango chake cha kula kila siku. Baada ya kusoma, tafakari na jiulize kama unafuata utaratibu huu kwa kuangalia kwa siku unakula nini zaidi na nini huli kabisa, kisha jiangalie na afya yako ikoje.

Matunda na mboga
Kundi la vyakula linalofuata kwa umuhimu ni matunda na mboga mboga. Tunatakiwa kula matunda ya aina mbalimbali, kwa sababu kila tunda lina faida na umuhimu wake katika mwili. Ingawa matunda ni mengi, lakini Mungu alivyopangilia, kila moja lina msimu wake.

Kwa kawaida, tunatakiwa kula matunda na mboga za majani kila siku, kiasi kisichopungua milo mitano. Lakini kwa bahati mbaya sana, siyo watu wote wenye fursa ya kupata na kula matunda kila siku. Hata wale wenye fursa hiyo, hawali inavyotakiwa.

Kitendo cha kutokula matunda hukosesha miili yetu virutubisho muhimu vya kujenga na kuimarisha kinga ya mwili, matokeo yake miili yetu inakuwa haina kinga ya kutosha. Mwili unapokuwa na kinga dhaifu, ni rahisi kushambuliwa na maradhi hatari, ikiwemo saratani, ambayo kinga yake kubwa iko kwenye ulaji wa matunda na mboga za majani.

Utashangaa kuona mtu anamaliza mwezi mzima hajala hata tunda moja. Msimu wa machungwa, kwa mfano, unaingia mpaka unaisha hajala hata chungwa moja. Ukija msimu wa maembe nao ni hivyo hivyo. Kuna mazoea ya kuona matunda siyo sehemu ya vyakula muhimu. Tabia hii ndiyo chanzo cha magonjwa mengi yanayotukabili hivi sasa.

NJIA SAHIHI YA KULA MATUNDA
Kwa upande mwingine, kuna makosa hufanyika wakati wa kula matunda. Kitaalamu inashauriwa kula matunda tumbo likiwa tupu, yaani kabla hujala kitu chochote tanguliza matunda kwanza na baada ya nusu saa au saa moja, ndiyo unashauriwa ule mlo wako kamili.

Lakini kanuni hiyo imekiukwa, tena hata katika mahoteli makubwa ambayo yana wapishi wanaoaminika kujua masuala ya lishe. Ni jambo la kawaida watu kuanza kula chakula na baadaye matunda (desert).

Itaendelea wiki ijayo.

2 comments:

Anonymous said...

Umeshauri huu ni hazina muhimu sana kwa jamii.Asanteni sana.

Disminder orig baby said...

kaka asante sana.