Katibu
Mtendaji wa BASATA, Ghonche Materego akizungumza na wadau wa Jukwaa la
Sanaa kuhusu umuhimu wa Sanaa za Asili wakati Kikundi cha Ngoma za Asili
cha Chabwede kutoka Kijiji cha Makumbusho ya Taifa kikitumbuiza. Kulia kwake ni Katibu wa Kundi hilo, Anna Said Tindima.
Katibu
wa Kundi la Chabwede, Anna akiwaleza Wadau wa Jukwaa la Sanaa juu ya
hatari ya kufifia kwa ngoma za asili kutokana na Vijana wengi kuipa
kisogo fani hiyo.
Akina
mama wapiga ngoma kwenye Kundi la Chabwede wakiwajibika vilivyo wakati
wakitoa burudani kwenye Jukwaa la Sanaa la BASATA wiki hii.
Wacheza
ngoma wa Kundi la Chabwede wakionesha vitu vyao kwenye Jukwaa la Sanaa
linalofanyika kila Jumatatu makao makuu ya BASATA, Ilala Sharif Shamba.
Sehemu
ya wadau waliohudhuria Jukwaa la Sanaa wiki hii wakifurahia burudani
iliyokuwa ikiporomoshwa na Kundi la Ngoma za Asili la Chabwede.
Na Mwandishi Wetu
Baraza
la Sanaa la Taifa (BASATA) limewataka wasanii kujikita kwenye ngoma za
asili huku likitoa wito kwa wasanii wakongwe katika fani hiyo
kuirithisha kwa watoto.
Wito huo umetolewa wiki hii na Katibu Mtendaji wa Baraza hilo,
Ghonche Materego mara baada ya kushuhudia burudani ya kuvutia
iliyoporomoshwa na Kikundi cha Ngoma za Asili cha Chabwede kwenye Jukwaa
la Sanaa linalofanyika kila wiki makao makuu ya BASATA.
Alisema
kuwa, kwa sasa ngoma nyingi za asili zinateteleka kutokana na wasanii
kujikita kwenye fani nyingine au kujiingiza kwenye sanaa za kisasa hivyo
kuhitajika juhudi za makusudi katika kurithisha sanaa hii kwa watoto
lakini pia wasanii kutumia vionjo vya asili katika kazi zao.
“Hapa
tumeambiwa ngoma kama za Segere na Mdundiko zinaanza kupotea, ni lazima
vikundi vya ngoma vihusishe watoto ili waweze kurithi” alisema
Materego.
Aliongeza kuwa, kuna
haja ya wasanii kuanza kujiuliza na kuzijaribu ngoma za asili kwenye
kazi zao, ili kuona ni kwa kiwango gani zinatofautiana kutoka eneo moja
hadi jingine lakini pia kuleta vionjo tofauti katika kazi zao.
Katika kuunga mkono harakati za Kundi la Chabwede katika kukuza fani ya ngoma za asili, BASATA ilitoa ngoma tatu za kisasa.
“BASATA
tunatambua juhudi za kundi hili, katika kuliunga mkono zaidi na
kuungana nalo katika kazi zao, tunalipatia ngoma tatu za kisasa”
aliongeza Materego.
Awali
akizungumza na Wadau wa Jukwaa la Sanaa baada ya kutoa burudani, Katibu
wa Kundi hilo linalofanya kazi zake eneo la Kijiji cha Makumbusho Anna
Said Tindima alisema kuwa, kwa sasa vijana wengi wamekuwa wakidharau
ngoma za asili hali inayodidimiza fani hiyo.
Aliongeza
kuwa, kuna kila sababu ya vijana kurudi kwenye asili zao na kujihusisha
kikamilifu na sanaa zinazopatikana maeneo yao ili kuhakikisha
hazipotei.
No comments:
Post a Comment