Tuesday, July 17, 2007

WALIOMUUA AMINA KAZI KWAO!


Na Makongoro Oging
Kamanda wa polisi Mkoa wa Kinondoni Bw. Jamal Rwambow ametoa msimamo wa jeshi lake kuwa watawakamata na kuwahoji wale wote wanaodaiwa kumuua aliyekuwa mbunge kupitia Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) marehemu Amina Chifupa endapo watapata taarifa yenye ushahidi juu ya kifo hicho.

Akizungumza na mwandishi wetu juzi kwa njia ya simu Kamanda Rwambow alisema kuwa endapo baba wa marehemu atakuwa dira kwa kuwakilisha majina ya watu wanaosadikiwa kuhusika na kifo hicho watayapokea na kuyashughulikia kisheria.

"Sisi polisi mkoa wa Kinondoni hatujapokea malalamiko hayo lakini wanafamilia wakilalamika na kutuletea majina hayo tutayafanyia kazi," alisema Rwambow.

Aidha aliendelea kusema kuwa endapo kuna watu wengine licha ya baba wa marehemu wanawajua waliohusika na kifo hicho watoe taarifa polisi ili sheria ichukue mkondo wake.

Kamanda huyo aliyasema haya kufuatia tamko la mzee Chifupa hivi karibuni alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari katika ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo kuwa, kifo cha Amina kimetokana na wabaya wake hasa wanaofanya biashara za dawa za kulevya ambapo marehemu alikuwa akipiga vita biashara hiyo.

Mzee Chifupa alizidi kusema kuwa licha ya wasiwasi uliotanda kuwa mwanae kifo chake kinaweza kutokana na wabaya wake pia alikuwa na msongo wa mawazo, kisukari ambacho kilifikia 400 na homa, na kuongeza kuwa wakati Amina akiwa Hospitali ya Lugalo alikuwa akizungumza maneno ya ajabu na mazito yakiashiria kifo chake.

Aidha alisema marehemu aliacha majina 26 ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya ambao hata hivyo hakuyataja bali aliwaomba wananchi wenye ushahidi wowote uliosababisha kifo cha mtoto wake iwe kwa sumu au kurogwa waieleze serikali ichukue hatua na kuwakamata wahusika, baadaye wajulishwe wanandugu na wako tayari kupokea taarifa hizo ziwe nzuri au mbaya.

Mzee Chifupa ametoa ombi kwa serikali kuwa ikiwa yupo kiongozi yeyote au mwananchi ametajwa katika biashara hii ya dawa za kulevya awekwe hadharani hata akiwa mmoja wa wanafamilia yao au akiwa mbunge au mjumbe wa NEC atajwe bila kujali kama muhusika yupo serikalini au popote pale Duniani.

'Serikali isiwe na kigugumizi kwa hili ikiwa viongozi au wahusika wanatuharibia Taifa letu kwa nini tuwaache, askari akiwa vitani na kukimbia vita hatua kali huchukuliwa dhidi yake hata kama askari huyo anajulikana kupita kiasi "alisema mzee Chifupa.

Hata hivyo, baadhi ya wananchi waliohojiwa jijini Dar es Salaam wamesema kuwa hakuna sababu ya mzee Chifupa kukalia majina ya vigogo wa dawa za kulevya hivyo kupewa wito wa kuyapeleke polisi ili yafanyiwe kazi.


BALAA LA BALALI

Elvan Stambuli na Dotto Mwaibale

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Daudi Bilali anazidi kukumbwa na balaa baada ya juzi, kiongozi wa chama cha siasa cha DP, Mchungaji Christopher Mtikila kudai kwamba ni lazima atampandisha kizimbani.

Mtikila alisema atafanya hivyo kutokana na tuhuma nzito ambazo kiongozi huyo wa benki anakabiliwa baada ya kuibuliwa bungeni hoja ya ufujaji wa fedha za taasisi hiyo nyeti ya umma.

Aliongeza kuwa anawajua wale wote walioshiriki kufuja fedha hizo wakiwemo wafanyabiashara wakubwa (majina tunayahifadhi) aliodai wamechezea mabilioni ya fedha za nchi yetu ambayo ni ya tatu kwa umasikini duniani.

Awali baadhi ya wabunge walidai kuwa kuna mtandao unaotawanya habari kuwa Benki Kuu ya Tanzania ilitumia fedha nyingi kuliko inavyostahili, kujenga ghorofa mbili ambapo shilingi bilioni 40 inadaiwa zilifunjwa kupitia akaunti ya madeni ya nje.

Inadaiwa fedha hizo zililipwa na maofisa wa BoT kwa kushirikiana na wanasiasa waandamizi pamoja na wafanyabiashara wakubwa.

Baadhi ya watu walioongea na mwandishi wetu kwa nyakati tofauti kufuatia kuwepo kwa madai ya matumizi hayo mabaya ya pesa kupitia BoT walikuwa na haya ya kueleza:-

Bw.Ali mkazi wa vingunguti alisema kwamba anasikitika sana pale Benki kuu inapodaiwa kufuja fedha na kumkopesha Mbunge wa Kwela Mhe.Chrisanti Mzindakaya shilingi Bilion 9 huku kukiwa na watu wengi wakiathirika na ugumu wa maisha.

Mkazi mwingine wa Chanika Bw. Augustino John, alisema kwamba Benki kuu imekuwa ikiwathamini zaidi viongozi na wafanyabiashara wakubwa huku wakisahau kuwa kuna wananchi walio wengi maeneo mbalimbali nchini wanaishi kwa mlo mmoja tu.

Bw. Mafuru mkazi wa Mombasa Ukonga alisema kwamba kama kweli kuna ufujaji wa fedha BoT, basi nchi inakwenda kubaya na kuhoji je pesa nyingi kama kweli zimefujwa nchi hii tunaipeleka wapi.

Naye Bw. Musa Saluo alisema kwamba inatakiwa Benki Kuu kuweka wazi mikataba ya utoaji pesa ili kuepuka mambo au tuhuma kama hizi zilizozagaa sasa zisitokee tena.

Akihutubia Bunge Julai 2, mwaka huu, Waziri Mkuu Bw. Edward Lowassa alisema serikali imechukizwa na kupotea kwa fedha ndani ya Benki Kuu na wamechukua hatua.

Alisema wamemuagiza Mkaguzi na Mthibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa kushirikiana na wakaguzi wa Kimataifa kuchunguza tuhuma hizo na kwamba jambo hilo halihitaji kuundwa kwa kamati teule ya Bunge.

3 comments:

Anonymous said...

Bwana Abdallah, mimi nina swali. Nataka nifahamu kama "KWA MFANO" kifo cha Mh.Amina Chifupa kikiwa kimetokana na kurogwa, sasa watu waliomroga watakamatwa vipi? ushahidi utakuwepo kweli? kumbuka kwamba tunaongelea mambo ya ulimwengu wa giza.(ulimwengu usioonekana katika macho ya ki binadamu).KESI ITAKUWAJE???

Anonymous said...

Ndugu Mrisho nashukur kwa kuskilza malalamiko yangu na kuyafanyia kazi,mimi ni mdau niliesema jana mbona unatupa vichwa vya habari tu?na sio kama mwanzo ulikuwa ukitupa habari kamili,Hivo asante kwa kuniskiliza au kutuskiliza wadau.

Anonymous said...

MMEMUUA NYIE NA UDAKU WENU